Revelation of John 22

1Kisha malaika akanionesha mto wa maji ya uzima, maji yalikuwa ya mng’ao kama wa bilauri. Yalikuwa yakitiririka kutoka katika kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana Kondoo 2Kupitia katikati ya mtaa wa mji. Katika kila pembe ya mto palikuwa na mti wa uzima, unaozaa aina kumi na mbili za matunda, na huzaa matunda kila mwezi. Majani ya mti ni kwa ajili ya uponyaji wa mataifa.

3Wala hapatakuwa na laana yoyote tena. Kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana Kondoo kitakuwemo ndani ya mji, na watumishi wake watamtumikia. 4Watamuona uso wake, na jina lake litakuwa juu ya vipaji vya nyuso zao. 5Hapatakuwa na usiku tena; wala hapatakuwa na hitaji la mwanga wa taa au jua kwa sababu Bwana Mungu ataangaza juu yao. Nao watatawala milele na milele.

6Malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kuaminika na kweli. Bwana Mungu wa roho za manabii alimtuma malaika wake kuwaonesha watumishi wake kitakachotokea hivi karibuni.” 7“Tazama! Ninakuja upesi! Amebarikiwa yeye anayeyatii maneno ya unabii wa kitabu hiki.”

8Mimi, Yohana, ndiye niliyesikia na kuona mambo haya. Nilipoyasikia na kuyaona, nilianguka chini mwenyewe mbele ya miguu ya malaika kumwabudu, malaika aliyenionesha mambo haya. 9Akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi ni mtumishi mwenzako, pamoja na ndugu zako manabii, pamoja na wale wanaotii maneno ya kitabu hiki. Mwabudu Mungu!”

10Akaniambia, “Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, maana wakati umekaribia. 11Asiye mwenye haki, aendelee kutokuwa mwenye haki. Ambaye ni mchafu kimaadili, na aendelee kuwa mchafu kimaadili. Mwenye haki, na aendelee kuwa mwenye haki. Aliye mtakatifu, na aendelee kuwa mtakatifu.”

12“Tazama! Naja upesi. Ujira wangu uko pamoja nami, kumlipa kila mmoja kulingana na alichokifanya. 13Mimi ni Alfa na Omega, wa Kwanza na wa Mwisho, Mwanzo na Mwisho.

14Wamebarikiwa wale waoshao mavazi yao ili kwamba wapate haki ya kula kutoka katika mti wa uzima na kuuingia mji kupitia malangoni. 15Nje kuna mbwa, wachawi, wazinzi, wauwaji, waabudu sanamu, na kila apendaye na ashuhudiaye ushahidi wa uongo.

16Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia kuhusu mambo haya kwa makanisa. Mimi ni mzizi wa uzao wa Daudi, Nyota ya Asubuhi ing’aayo.”

17Roho na Bibi harusi asema, “Njoo!” Na yeye asikiaye aseme, “Njoo!” Yeyote aliye na kiu, na aje, na yeyote anayetamani, na apate maji ya uzima bure.

18Namshuhudia kila mtu asikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki: Kama yeyote ataongeza katika hayo, Mungu atamuongezea mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. 19Kama mtu yeyote atayaondoa maneno ya kitabu hiki cha unabii, Mungu ataondoa sehemu yake katika mti wa uzima na katika mji mtakatifu, ambayo habari zake zimeandikwa ndani ya kitabu hiki.

20Yeye ashuhudiaye mambo haya asema, “Ndiyo! Naja upesi.” Amina! Njoo, Bwana Yesu! 21Neema ya Bwana Yesu iwe na kila mtu. Amina.

Copyright information for SwaULB